Decolonial Travel Guide Tanzania

Ukoloni wa Kijerumani na Jinsi Unavyoathiri hali ya sasa katika Tanzania Bara

Reginald Elias Kirey

Tanzania Bara ya sasa ilikuwa sehemu ya koloni la zamani la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, lililojulikana kama Deutsch-Ostafrika. Koloni hili liliundwa na maeneo ambayo kwa sasa ni nchi za Rwanda na Burundi, na hivyo kuifanya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani kuwa koloni kubwa la takriban kilomita za mraba milioni moja. Mbio za Ujerumani za kutafuta makoloni Afrika ya Mashariki zilianza mwaka 1882 wakati Chama cha Ukoloni cha Kijerumani (Deutscher Kolonialverein) kilipoanzishwa na Reich (dola ya kifalme ya Ujerumani) kwa lengo la kuendeleza harakati za kupata makoloni ya ng’ambo. Ukoloni wa Ulaya kwa kiasi kikubwa ulisukumwa na mahitaji yao ya kiuchumi kwa ajili ya kupata malighafi kutoka Afrika, upatikanaji wa nguvu kazi rahisi na ya bei ya chini, ardhi pamoja na masoko.

Mwaka 1884, Carl Peters alianzisha Jumuiya yake ya Ukoloni wa Kijerumani (Society for German Colonisation) ambayo ilifanya mikataba ya uongo (bandia) – iliyojulikana kama “barua za dola ya kifalme za ulinzi”(imperial letters of protection) – na baadhi ya machifu wa Kiafrika katika maeneo kama Uzigua, Uluguru na Usagara. Kwa kusaini mikataba hiyo, machifu walidanganywa kuamini kuwa nguvu za kifalme zingelinda jamii au maeneo yao. Utaratibu huu ulimwezesha Peters kuanzisha koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, jambo ambalo liliwakera machifu waliokuwa hawakutarajia kabisa kutawaliwa na Wajerumani.

Mapambano ya Ujerumani ya kupata maeneo hayakupatikana tu kupitia mikataba, bali pia kupitia ushirikiano, kulazimisha, na matumizi ya nguvu za kijeshi (gunboat diplomacy). Mbinu hizi tofauti za Ujerumani za kutawala Afrika ya Mashariki ziliongezeka mara baada ya Kansela Otto von Bismarck kuidhinisha rasmi sera ya ukoloni tarehe 22 Februari, 1885. Vituo vya kijeshi vya Kijerumani vilianzishwa mara moja katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha udhibiti madhubuti wa kikoloni na kuimarisha ushawishi wa kifalme wa Kijerumani dhidi ya nguvu pinzani kama Waingereza.

Mapambano haya madogo yalitokea katika pwani na maeneo ya ndani ya Tanganyika. Pamoja na mapambano mengine ya makubwa kama Vita vya Maji Maji, vilivyolenga kupinga unyonyaji wa Kijerumani, vilikandamizwa barabara kwa nguvu za majeshi ya kikoloni ya Kijerumani (Schutztruppe). Baada ya kushindwa kuzuia nguvu ya Schutztruppe, baadhi ya machifu wa Kiafrika waliopinga ukoloni wa Kijerumani walikamatwa kama mateka wa kivita na hatimaye kuuawa. Mauaji haya yaliambatana na uporaji wa mali na kusafirishwa kwa mabaki ya binadamu kama vile fuvu la kichwa. Hadi leo, machifu hawa wanaheshimiwa kama mashujaa wa vita kwa sababu ya ujasiri wao wa kupinga utawala wa Kijerumani. Kwa mfano, sanamu zimejengwa maeneo mbalimbali nchini; aidha, barabara na taasisi za serikali kama shule na vyuo vikuu zimepewa majina yao.

Ukoloni wa Kijerumani haukubadilisha tu mamlaka ya jadi ya jamii za kabla ya ukoloni, bali pia ulianzisha vipengele vipya vya kijamii, kiuchumi na kitamaduni ambavyo havikuwa vya asili kwa wenyeji. Uchumi uliokuwa unastawi kabla ya ukoloni, pamoja na mahusiano yake ya kiuchumi na mtandao wa biashara wa Kiafrika uliokuwa umejengeka tayari, uliunganishwa katika mifumo ya uzalishaji na unyonyaji ya kibepari ya kimataifa. Unyonyaji wa Kijerumani ulionekana kwa namna ya kulazimisha wakulima walime mazao ya biashara kwa ajili ya kuuza nje; kufanya nguvu kazi kwa bei rahisi (cheap labour) katika migodi, mashamba ya wakoloni, na mashamba makubwa ya mashamba ya kilimo; ushuru wa kulazimishwa pamoja na kunyang’anya ardhi ya Waafrika ambayo hapo awali ilikuwa chini ya umiliki wa jadi. Zaidi ya hayo, maadili mapya ya kitamaduni kama elimu ya Magharibi, Ukristo, mitindo ya mavazi na ya chakula vililetwa katika jamii za Afrika Mashariki kwa ujumla (Tanganyika ikiwemo).

Usambara Bahn (c) ub-bildarchiv-dkg-uni-frankfurt / Wikimedia

Ingawa ukoloni wa Kijerumani katika Afrika ya Mashariki haukudumu kwa muda mrefu kwa kuwa mamlaka yake yalihamishwa kwa Waingereza na Wabelgiji mara baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, athari zake kijamii, kisiasa na kiuchumi ni za kudumu kwa watu wa Tanganyika.

Kwa mfano, mipaka mingi ya kisiasa au kijiografia iliyopo leo ilianzishwa wakati wa utawala wa Kijerumani, ukiachilia mbali jiji la Dar es Salaam ambalo liliendelea kuwa makao makuu ya kisiasa ya serikali hadi karibuni. Sekta ya kilimo ya sasa inatoa ushahidi wa urithi wa kiuchumi wa Kijerumani, kwani wakulima katika maeneo mbalimbali bado wanalima mkonge au kahawa ambazo ziliingizwa na wamisionari, wakoloni na wamiliki wa mashamba wa Kijerumani kama mazao ya biashara kwa soko la nje.

Miundombinu ya Kijerumani ni ushahidi mwingine wa jinsi ukoloni ulivyoendelea kuathiri maisha ya sasa Tanzania. Kwa mfano, muundo wa barabara kuu za mikoa na reli haujabadilika sana kutoka ule wa Kijerumani. Hali hiyo hiyo inajitokeza kwenye muundo wa mitaa ya miji ya kikoloni kama Dar es Salaam. Ingawa majina ya barabara yalibadilishwa baada ya uhuru, mifumo yake ilibaki kama ilivyokuwa. Vivyo hivyo, urithi wa usanifu majengo wa miji ya kikoloni na vituo vya wamisionari wa Kijerumani unaendelea kuathiri usanifu wa sasa wa majengo nchini Tanzania. Kwa sababu hiyo, majengo mapya ya utawala au ya kidini yanaonyesha vipengele vya usanifu wa majengo wa Kijerumani. Si ajabu kuwa Ikulu mpya ya serikali iliyojengwa Dodoma inafanana sana na Ikulu ya zamani ya Kijerumani iliyoko Dar es Salaam. Majengo kadhaa ya kikoloni ya Kijerumani yaliyopo sehemu mbalimbali nchini yametangazwa kuwa makumbusho ya kitaifa kutokana na thamani yake ya kihistoria, kiuchumi, kiutamaduni, na ya kuvutia. Majengo hayo yanalindwa na Sheria ya Mambo ya Kale Na. 22 ya mwaka 1979.

Kumbukumbu za kizazi hadi kizazi kuhusu tajiriba za ukoloni wa Kijerumani Tanganyika zimeunda sura mpya ya namna ya kukumbuka mambo mbalimbali pamoja na jambo la ushujaa mara baada ya ukoloni. Kwa mfano, kumbukumbu za pamoja za ukatili wa Kijerumani zimezalisha aina mbalimbali za ukumbusho wa mashujaa wa vita. Hali hii inaonekana katika matukio ya hivi karibuni ya ukumbusho wa kitaifa wa Vita vya Maji Maji pamoja na ujenzi wa makumbusho ya vita na makaburi (ya kihistoria). Matukio haya yameimarisha siasa za kurejesha mabaki ya binadamu, na kilele chake kilikuwa ziara ya Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika Makumbusho ya Maji Maji mjini Songea mnamo Novemba 2023, ambapo aliomba radhi kwa ukatili uliofanywa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Hivyo basi, ukoloni wa Kijerumani pia umeathiri maudhui ya mtaala wa historia unaotumika katika shule za msingi na sekondari. Historia ya Kijerumani inachukua nafasi kubwa katika historia ya ukoloni wa Tanganyika. Mada hizo zinahusu vita vya ukoloni, upinzani, unyonyaji, elimu, huduma za afya pamoja na uinjilishaji. Kwa ujumla, ukoloni wa Kijerumani wa Tanganyika ulileta athari kubwa kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kumbukumbu za pamoja za ukoloni wa Kijerumani haziishi tu kwenye urithi wa majengo na kitamaduni, bali pia zinaenezwa kupitia shule na matukio ya ukumbusho. Vile vile, haipaswi kusahaulika kwamba kumbukumbu za ukoloni wa Kijerumani pia zinaishi katika fikra za watu kupitia simulizi za kizazi hadi kizazi.

taarifa zaidi