Lena Luise Mattmüller
Baada ya kujitolea (kama volunteer) Tanzania mwaka 2022, nilipenda nchi hiyo mara moja. Ilikuwa wazi kwamba ningependelea kutumia muda nikiwa Dar es Salaam badala ya kurudi Ujerumani yenye baridi, nikitafuta kazi baada ya kipindi cha kujitolea. Hata hivyo, nilifahamu kwamba sijui mengi kuhusu historia ya Tanzania, hasa kipindi cha ukoloni wa Kijerumani. Kabla ya kurudi Februari 2023, niliamua kujitafakari na kujipa elimu kuhusu hilo. Pia nilitaka kutazama nchi kwa treni — njia ya reli iliyojengwa wakati wa ukoloni wa Kijerumani — ili kufuatilia alama/nyazo za wakati huo. Nilishawahi kusafiri Dodoma na Mwanza, lakini sikuwa najua vizuri kwamba vilianzishwa na Wajerumani, isipokuwa kwa majina kama Bismarck Rock Mwanza. Nilipanga safari hii kuangalia kwa makini alama/nyayo za ukoloni wa Kijerumani na kujilimbikizia maarifa kabla ya kuanza safari ya kujifunza kuhusu historia ya kikoloni.
Kuondoka Dar es Salaam
Baada ya kufanikiwa sio tu kukiona kituo cha treni jijini Dar es Salaam — kituo kikuu cha enzi za ukoloni kilichokuwa kinakarabatiwa — bali pia kupitia mchakato wa kununua tiketi, siku chache baadaye nilijikuta nimesimama mbele ya treni ya zamani ya Central Line, iliyokuwa ikijulikana kama Mittellandbahn, ambayo ilionekana kuwa mchanganyiko wa mabehewa ya aina mbalimbali. Niliketi daraja la pili, katika behewa la kulala. Ingawa behewa langu lilikuwa limepangwa kwa wanawake sita, hili lilijumuisha pia watoto wao. Hivyo tulikuwa watu kumi ndani ya chumba kidogo, pamoja na mizigo na chakula kwa safari ya siku mbili kwa treni.
Kitu kilichonivutia zaidi ni majengo ambayo treni ilipita kwa mwendo wa polepole — ambayo kwa wazi yalikuwa ya enzi za Wajerumani. Wakati awali nilikuwa na ugumu kutambua majengo ya kikoloni ya Kijerumani, safari hii nilianza kutambua zaidi na zaidi mtindo wa Kijerumani katika vituo vya treni. Katika kituo kimoja, hata neno la Kijerumani “Halt” liliandikwa kwenye bango kubwa, na kwenye moja ya magofu ambayo treni ilipita karibu nayo, niliweza kusoma neno la Kijerumani “Speisehaus” (nyumba ya chakula/mgahawa).
Kuwasili Kigoma
Baada ya safari ya karibu saa 45, tulifika Kigoma, mji ulioko magharibi mwa Tanzania kandokando ya Ziwa Tanganyika. Ziwa hili linachukuliwa kuwa moja ya maziwa ya zamani na yenye kina kirefu zaidi duniani. Kituo kizuri cha reli cha enzi za ukoloni — ambacho pia ni mwisho wa reli — kilijitokeza mbele yetu kwa fahari. Kutoka ndani ya treni, tayari niliweza kuona kituo changu kinachofuata : Liemba, meli ya kivita ya zamani ambayo Ujerumani iliisafirisha hadi Ziwa Tanganyika wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia kwa kutumia reli hiyohiyo niliyopitia hadi Kigoma. Nilikuwa nimegundua hapo awali kuwa meli hiyo ilijulikana kwa jina la Kijerumani “Götzen” wakati huo. Kwa kuwa sikuweza kupata taarifa za hivi karibuni kuhusu Liemba, nilifurahi sana kuona kwamba meli hiyo bado ipo bandarini. Baada ya kuwalipa wafanyakazi wa bandari “ada ya kuingia,” niliruhusiwa kwenda kizimbani na kuonyeshwa maeneo mbalimbali ndani ya meli hiyo. Huko nilijifunza kuwa Liemba inatarajiwa kukarabatiwa ili iweze tena kusafiri hadi Zambia kama meli ya abiria, kama ilivyofanya kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita. Siku zilizofuata nilizitumia Kigoma katika kutembelea kasri la uwindaji la Kaisari Wilhelm. Mwongoza wangu wa Liemba alikuwa tayari amenitambua kama mtu mwenye nia ya waziwazi kuhusu meli hiyo, lakini hakuweza kuelewa kwa nini watu “kama mimi” walivutiwa na mtumbwi wa kutu kama huo.
Vituo vya Njiani Tabora, Dodoma, na Iringa
Katika safari yangu ya kurudi Dar es Salaam, nilisafiri kwa basi na kufanya vituo vyaTabora na mji mkuu Dodoma — maeneo mawili yaliyokuwa vituo vya utawala wa kikoloni wa Kijerumani. Mji mkuu huu, ulioko katikati ya nchi, ulianzishwa mwaka 1907 na wakoloni Wajerumani, lakini hata huko — kama ilivyokuwa Tabora, ambalo liligeuka kuwa kituo cha biashara kwa Wajerumani kutokana na ujenzi wa reli — kutafuta mabaki ya enzi za ukoloni kulikuwa jambo gumu. Sikuweza kutambua majengo au maeneo muhimu ya enzi za ukoloni kwa kutumia maarifa yangu madogo ya historia pamoja na utafiti wa mtandaoni. Hali hii ilibadilika Iringa tu, katika nyanda za juu za kusini mwa Tanzania. Asili ya mji huo ilikuwa matokeo ya moja kwa moja ya Vita vya Wahehe, vilivyotokea kati ya mwaka 1891 na 1898, hasa katika eneo la Iringa na maeneo ya jirani. Wahehe, watu waliokuwa chini ya uongozi wa Chifu Mkwawa, walipigana — na hatimaye kushindwa — dhidi ya wakoloni Wajerumani. Makumbusho na maeneo muhimu jijini bado yanakumbusha tukio hilo hadi leo. Ziara zilizoongozwa katika Boma iliyojengwa mwaka 1894 zilikuwa na taarifa nyingi muhimu. Ziara hizo ziliwasilisha mchanganyiko wa kuvutia wa historia ya kikoloni na utamaduni wa kienyeji wa Wahehe, jamii inayojulikana kwa ngoma zake, muziki, na ufundi wa jadi.
Kutoka Kaskazini kuelekea Moshi na Arusha
Katika safari zangu za baadaye kwa treni, kupitia reli ya kwanza kabisa nchini Tanzania — Reli ya Usambara — ambayo hapo awali ilikuwa ikiishia Moshi kwenye kituo chake cha Kijerumani, bado niliweza kuona athari za enzi za ukoloni. Katika jiji la kitalii la Arusha, pia kulikuwa na makumbusho ndani ya Boma ya zamani, yenye maonyesho kuhusu enzi za ukoloni. Hata treni ya kisasa ya mwendo kasi ya SGR (Dar – Dodoma), iliyozinduliwa mwaka 2024, inafuata njia ileile ya reli ya Kijerumani ya kikoloni na inatumia mabehewa ya ghorofa mbili ya zamani kutoka Deutsche Bahn ya Ujerumani.
Mwisho wa safari yangu uliniacha na hisia mseto za mshangao — mshangao juu ya jinsi gani Tanzania bado imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na utawala wa kikoloni wa Kijerumani, iwe ni katika miundombinu ya miji au usafiri. Na pia mshangao juu ya jinsi ambavyo maarifa haya hayapo sana nchini Ujerumani. Ni ukweli kuwa, mshangao huo uligeuka kuwa aibu kwa kutojua kwangu kuhusu mabaki au nyayo hizi za utawala wa Kijerumani, ambayo Watanzania huona na kutumia kila siku. Majengo, hadithi, reli na majina kutoka enzi ya ukoloni wa Kijerumani bado yanaishi Tanzania, ilhali vilikuwa vimejificha kwa muda mrefu — na mara nyingi vinaendelea kubaki hivyo.









