Decolonial Travel Guide Tanzania

Kumbukumbu za Ukoloni wa Deutsch-Ostafrika Nchini Ujerumani

Henriette Seydel

→ Maeneo ya Ukoloni Nchini Ujerumani

Urithi wa ukoloni unaendelea kuathiri Ujerumani hadi leo. Tamaduni za kukumbuka huu urithi zimebadilika sambamba na matukio ya kisiasa ya ndani.

1918–1933:  muda wa michakato ya Exoticization (uonaji wa mambo ya kigeni hasa afrika kuwa ni duni na ajabu) and revisionism (ubadilishaji wa mambo)

Kupitia Mkataba wa Versailles wa mwaka 1919, Ujerumani ilipoteza makoloni yake kwa Mataifa Washirika. Ndani ya Ujerumani, jambo hili liliitwa “uongo wa hatia ya ukoloni” (colonial debt lie) – msemo wa harakati za kikoloni za kutaka marejeo. Wakati huo huo, haiba ya vitu vya kigeni na biashara vilistawi kupitia maonyesho ya watu (Völkerschauen) na maduka ya bidhaa za kikoloni, yaliyokuwa na matangazo ya kibaguzi ya kahawa, chokoleti na pombe ya rum. Ripoti za safari, riwaya na filamu ziliromantisha urithi wa kikoloni kama wa kishujaa na wa kusisimua. Sanamu za ukumbusho zilijengwa na barabara zilizopewa majina ya “mashujaa wa ukoloni” kama Hermann von Wissmann au Paul von Lettow-Vorbeck.

1933–1945: Ushujaa wa Kikoloni (colonial heroism) na Ubaguzi wa Rangi

Mwaka 1939, sanamu la ukumbusho wa askari wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani lilijengwa Hamburg, likiwaonyesha Paul von Lettow-Vorbeck na Askari. Katika Jamhuri ya Weimar kumbukumbu hii ilisahaulika au kufichwa, lakini katika Ujerumani ya Wanazi, Carl Peters alirudishwa na kutambulishwa upya. Mtawala huyu wa kikoloni mwenye ukatili alisifiwa kama mfano bora wa uanaume wa Kijerumani, ujasiri na ubwana wa Mzungu. Waimperialisti walitaka urejeshwaji wa makoloni na waliota kuhusu “Afrika ya Kati ya Kijerumani” kama eneo jipya la makazi, vyanzo vya malighafi, masoko na chanzo cha wafanyakazi. Kwa Wanazi (National Socialists), lengo lilikuwa kwanza kupanua “Lebensraum” (eneo la kuishi) huko Ulaya Mashariki. Uwepo wa watu Weusi na wa Asia ndani ya Dola ya Ujerumani – kama wahamiaji wa kikoloni waliokuwa Askari, wanafunzi wa misheni, wasanii, wanamuziki, au Wajerumani Weusi – ulionyesha historia hiyo ya kikoloni. Kwa msingi wa itikadi ya ubaguzi wa rangi iliyokuwa ikifundishwa hata kabla ya Wanazi, watu wasio Wazungu walibaguliwa, kutengwa, kunyimwa haki na kuuawa kwenye kambi za mateso1 .

1945–1967: Ushirikiano wa Mashariki na Magharibi ya Ujerumani na Tanganyika

Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, mjadala wa kina kuhusu historia ya ukoloni haukupewa uzito, na mitazamo ya kibaguzi iliendelea. Katika Ujerumani Mashariki (DDR), lawama kwa ukandamizaji wa kikoloni zilipelekwa kwa Ujerumani Magharibi. Sanamu za kikoloni zilibomolewa na harakati za ukombozi Afrika ziliungwa mkono kama sehemu ya mapambano ya kimataifa ya wafanyakazi. DDR iliendeleza ushirikiano wa kiutamaduni, kiuchumi na kielimu na Tanganyika, na pia kuwa na ushawishi kwenye ujasusi wa Zanzibar, uliotumia mbinu kama za Stasi. Katika Ujerumani Magharibi (BRD), vyombo vya habari, filamu na matangazo vilijenga picha ya Afrika kama bara la njaa, umaskini na utegemezi. Kupitia kauli mbiu ya “msaada wa maendeleo,” miradi ya miundombinu na kiuchumi ilifadhiliwa, huku BRD ikiwa mfadhili wa tatu mkubwa kwa Tanganyika hadi 1964.

1968–1990: Mshikamano na nolstajia

Harakati za mwaka 1968 na zile za mshikamano na Dunia ya Tatu zilipinga mambo yaliyofichwa na historia ya ukoloni. Mahusiano na wanafunzi kutoka Kusini mwa Dunia yalichangia kwa mjadala kuhusu urithi wa kikoloni. Miji kadhaa ya Ujerumani Magharibi iliongeza mabango ya ukosoaji kwenye sanamu za kikoloni au kuzibadilisha kuwa alama za maonyo. Hata hivyo, mitazamo ya kupinga ukoloni ilibakia zaidi kwenye jamii za kiraia – hasa kwa diaspora na jamii za Wajerumani Weusi. Wengi wa watu waliisahau au kuikumbuka hiyo historia ya kikoloni kwa nolstajia yake tu. “Utalii wa Dunia ya Tatu” ulianza kuimarika. Ushirikiano wa maendeleo ulioanzishwa tena ulianza kupingwa kwa sababu ya miradi iliyokwama, madeni, matatizo ya lugha, na fursa zilizowekwa mbali kwa wataalam wazawa.

1990–2004: Amnesia ya kikoloni na Ukosoaji wake

Baada ya muungano wa Ujerumani, siasa kuhusu Afrika haikupewa kipaumbele. Ujerumani ilijiona haijachafuka sana na historia ya ukoloni – hali inayojulikana kama “Amnesia ya kikoloni.” Filamu na riwaya kuhusu Afrika zilirejea katika miaka ya 2000, lakini kwa mtazamo wa Afrika kama sehemu ya ndoto ya asili na vituko, si kama mjadala wa kihistoria. Mwaka 2004, Waziri wa Maendeleo Wieczorek-Zeul aliomba radhi kwa jinai za ukoloni nchini Namibia – hatua ambayo serikali ilijitenga nayo baadaye ili kuepuka madai ya fidia. Hotuba hii ilionyesha mjadala unaoendelea wa kupinga ukoloni katika jamii na vyuo vikuu.

2005–2025: Michakato ya kujikwamua na ukoloni na Ukoloni Mamboleo

Mwaka 2005, wakati wa kumbukumbu ya Mkutano wa Berlin na miaka 100 ya Vita vya Maji Maji, hakukuwa na wawakilishi wa serikali waliokuwepo. Wadau wa kiraia wa Kijerumani na Watanzania – wa kidini, kielimu na kijamii – ndio waliolileta suala la ukoloni mezani. Hadi leo, mashirika ya kiraia, harakati za baada ya ukoloni, jumuiya za watu Weusi, BiPoC, na watafiti wanaendesha kazi ya elimu na kupinga ubaguzi. Wanaandaa matembezi mijini, usomaji wa vitabu, maonyesho ya filamu, midahalo, maandamano, miradi ya sanaa, filamu, makala na vitabu – pamoja na kushinikiza mabadiliko ya majina ya barabara na urejeshaji wa mali za kihistoria. Pia sekta ya sanaa na utamaduni imejumuisha mada hii: makumbusho, maonyesho, miradi ya dansi au maigizo. Idadi ya miradi ya pamoja ya utafiti kama Humboldt Lab au ushirikiano kati ya Ujerumani na Rwanda juu ya mabaki ya binadamu kutoka Rwanda na Tanzania inaonyesha mabadiliko ya kimtazamo kuhusu ushirikiano wa kimataifa.

Wakati huo huo, kuna watu wanaofuata mtazamo wa kikoloni wa kurejesha kumbukumbu, wanaoenzi wanajeshi wa Kijerumani waliouawa, wanaopunguza ukali wa uhalifu wa ukoloni, wanaokusanya vitu vya zamani kama stempu na silaha, au wanaonunua bidhaa na samani za “mtindo wa kikoloni” kwa hisia za kihisia za “enzi nzuri zilizopita.” Vyombo vya habari, matangazo ya utalii barani Afrika, au miradi ya maendeleo mara nyingi bado vinaendeleza mitazamo ya kibaguzi, urithi wa kikoloni na mitazamo ya Ulaya kuwa kitovu cha dunia.

Baada ya uchaguzi wa Bunge la Ujerumani wa 2018, mada ya ukoloni ilitajwa kwa mara ya kwanza kwenye mkataba wa muungano wa kisiasa – ikielezwa kuwa urithi wa kikoloni, sambamba na historia ya DDR na Ujerumani ya Wanazi, unapaswa kupata nafasi kwenye kumbukumbu za taifa. Mwaka 2023, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliomba msamaha kwa vitendo vya ukatili wa kikoloni wakati wa ziara yake Tanzania. Hata hivyo, bado hakuna makumbusho ya historia ya ukoloni, siku za kitaifa za ukumbusho, wala mnara mkuu wa kumbukumbu kwa wahanga wa ukoloni wa Kijerumani.

Maeneo ya Ukoloni Nchini Ujerumani

Hannover: Sanamu la Carl Peters

Sanamu la Carl Peters lililojengwa mwaka 1930 liliongezewa jiwe la ukumbusho wa kukemea ukoloni mwaka 1988 baada ya mjadala mrefu. Maandishi ya awali “Mtu mkubwa wa saxony ya chini (Niedersachsen) Carl Peters, aliyetuletea Deutsch-Ostafrika” yalifunikwa. Wanaharakati wanapigania liondolewe kabisa.

Bad Lauterberg: Sanamu la Wissmann

Katika mji alikozaliwa pia kuna sanamu ya Wissmann. Kundi la Göttingen Postkolonial linapigania ukosoaji wa kazi hii, kwani maandishi “kwa Mwafrika mkuu” si ya kweli – sanamu hiyo bado ipo kwenye bustani ya mji huo.

Hamburg: Bustani ya Tanzania na Sanamu la Askari wa Deutsch-Ostafrika

Kwenye eneo la zamani la kambi ya kijeshi ya Lettow-Vorbeck, kuna bustani inayoitwa “Tanzania Park” yenye sanamu ya kumbukumbu ya wanajeshi wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hadi mwaka 1990, wanajeshi waliendelea kufunzwa hapa. Bustani na sanamu vinajadiliwa vikali hadi leo.

Munich : Barabara ya Tanga

Katika jiji hili la Bavaria, na pia Cologne na Berlin, kuna barabara zilizopewa jina kutokana na “Vita vya Tanga”. Mwaka 1914, Wajerumani walishinda dhidi ya wanajeshi wa Uingereza na India. Jenerali Paul von Lettow-Vorbeck alisifiwa kama shujaa. Ukweli kwamba mamia ya maelfu ya Waafrika — wanajeshi Askari na wakazi wa pwani ya Afrika Mashariki, walikufa kutokana na mapigano haya ulipuuzwa.

Berlin: Mabadiliko ya Jina la Barabara ya Petersallee

Baada ya miongo ya juhudi za kiraia, hasa kutoka kwa jamii ya Waafrika/Weusi, Petersallee (iliyopatiwa jina na Wanazi mwaka 1939) ilibadilishwa kuwa Maji-Maji-Allee na Anna-Mungunda-Allee – ikiheshimu harakati za Maji Maji na mwanamke shujaa wa kupinga ubaguzi kutoka Namibia.

Würzburg: Miamba ya Bismarck

Katika kuadhimisha miaka 50 ya ushirikiano kati ya Mwanza na Würzburg, mnamo 2016 ilijengwa nakala ya miamba ya Bismarck ya Mwanza. Wakosoaji wanataka jina libadilishwe – Mwanza na Würzburg – ili Bismarck, aliyekuwa muasisi wa ukoloni wa Afrika, asienziwe tena.

  1. Mfano mmoja ni Askari Bayume Mohamed Husen, ambaye alifanya kazi nchini Ujerumani kama mwigizaji wa filamu na mwalimu wa lugha ya Kiswahili kabla ya kuuawa katika kambi ya mateso ya Sachsenhausen. Mnamo 2007, Stolperstein (bamba la ukumbusho lililowekwa ardhini) liliwekwa kwa ajili ya Husen huko Berlin-ya kwanza kwa mwathirika Mweusi wa utawala wa Nazi. ↩︎