Decolonial Travel Guide Tanzania

Kusafiri kwa Njia Endelevu na salama– Lakini ni kwa njia gani?

Alien Spiller

Uendelevu sasa ni mojawapo ya maneno makuu katika sekta ya utalii na hulenga moja kwa moja mahitaji ya watumiaji. Kwa mujibu wa World Economic Forum, asilimia 86 ya wasafiri vijana hutamani ofa rafiki kwa mazingira. Hata hivyo, hali halisi mara nyingi ni tofauti: mitazamo ya kimazingira haimaanishi kuwa tabia pia ni endelevu. Aidha, baadhi ya huduma zinazodai kuwa endelevu si rafiki kwa mazingira wala kwa jamii – mara nyingi hubakia kuwa mbinu tu ya uuzaji iliyojaa ujanja.

Wakati huo huo, janga la COVID-19 lilipelekea watu wengi kuacha kabisa kusafiri, na hivyo kuongeza hamu ya kusafiri kwa wingi baadaye. Haishangazi basi kuwa hadi mwishoni mwa mwaka 2024, utalii wa kimataifa ulikuwa karibu kufikia kiwango cha kabla ya janga – yaani, wasafiri wa kimataifa wapatao bilioni 1.4. Kwa maeneo mengi ya utalii, hasa yaliyo Kusini mwa Dunia, hali hii ni habari njema. Kwa mtazamo wa maendeleo, utalii huonekana kama kichocheo cha ajira na uchumi. Wakati wa janga, zaidi ya nafasi milioni 60 za ajira zilipotea katika sekta ya utalii – hali iliyoleta madhara ya muda mrefu kwa wafanyakazi na miundo ya kijamii ya maeneo ya wenyeji. Kuanzishwa tena kwa safari ni nafasi si tu ya kurejesha ajira, bali pia kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha mishahara ya haki. Kuufanya utalii kuwa wa haki kijamii ni jambo la msingi, kwani hapo awali sekta hii ilichochea hali nyingi za ajira za mashaka.

Mbali na mazingira bora ya kazi, utalii endelevu unamaanisha kuwa mnyororo wa thamani ya utalii haunufaishi tu makampuni makubwa, bali pia biashara na jamii za wenyeji zinapaswa kufaidika kwa usawa. Uendelevu wa kitamaduni unamaanisha kuwa utalii haupaswi kuchangia kugeuza au hata kusukuma pembeni tamaduni za kienyeji au asili. Hatimaye, utalii ni lazima pia uwe wa kimazingira. Changamoto kubwa zaidi hapa ni usafiri wa anga: safari za ndege husababisha takriban asilimia 9 ya uzalishaji wa gesi chafu duniani. Hili linaonyesha mgongano mkubwa kati ya maendeleo ya kiuchumi na ulinzi wa hali ya hewa. Hata hivyo, wasafiri wanaweza kufanya maamuzi ya makusudi: kupunguza idadi ya safari za ndege, kukaa muda mrefu zaidi katika sehemu moja, kutumia njia mbadala endelevu za usafiri – kama vile treni, kutembea kwa miguu au kutumia baiskeli.

Kuchagua makampuni na waandaaji wa safari waliothibitishwa huimarisha viwango vya kijamii na kimazingira. Kusafiri kwa njia halisi kunamaanisha kutumia huduma na rasilimali za eneo husika na kupunguza athari za kimazingira kulingana na hali ya huko – hasa katika matumizi ya maji, kwani maeneo mengi ya likizo hukumbwa na uhaba wa maji. Sisi wa Tourism Watch tunaamini kuwa dunia yenye amani, haki na bila umaskini haiwezekani bila mabadiliko ya msingi katika sekta ya utalii. Haki za binadamu na uhuru wa kujiamulia wa jamii za wenyeji vinapaswa kuwa kiini cha kila mpango wa utalii. Manufaa ya kiuchumi na kijamii yanapaswa kusambazwa kwa haki, ili kuboresha ustawi na ubora wa maisha kwa wenyeji. Kwa maana hiyo, utalii unapaswa kuwa uzoefu chanya na wenye maana kwa wasafiri na jamii zinazowakaribisha.

Taarifa zaidi


Utalii endelevu ni wa haki ya kijamii, wenye usawa kiuchumi, unaoheshimu tamaduni, na ambao ni Rafiki wa kimazingira. Ni hatua gani tatu mahususi za uendelevu utazochukua kwa safari yako ijayo kwenda Tanzania au mahali pengine?