Decolonial Travel Guide Tanzania

Bagamoyo: Makumbusho la Kihistoria la Kikatoliki

Takriban kilomita mbili kaskazini-magharibi mwa kituo cha mji kuna Misheni ya Kikatoliki yenye jumba la makumbusho la kihistoria linalofaa kutembelewa. Linaonesha ushahidi wa kusikitisha wa historia ya utumwa, linaelezea historia ya umisheni na linatoa mwanga kuhusu kipindi ambacho Bagamoyo ilikuwa mji mkuu wa koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Mwaka 1868, utumwa katika Afrika ya Mashariki ulifikia kilele chake. Kati ya 1860 na 1870, takribani Waafrika 700,000 walitekwa nyara na kufanywa watumwa. Bagamoyo ilikuwa kituo cha mwisho barani kabla ya watu hao kupelekwa Zanzibar kuuzwa. Ndipo jina la mji huu lilipotokana – “Bwaga moyo” – likimaanisha “weka moyo chini”, kuonyesha huzuni kuu ya watumwa waliokuwa wakilazimishwa kuagana na maisha yao ya zamani. Ili kupambana na utumwa, wamisionari wa Kikatoliki wa Shirika la Roho Mtakatifu walianzisha kituo Bagamoyo mwaka 1868. Walinunua uhuru wa watumwa kadri walivyoweza na kuwasettle katika “Kijiji Huru cha Kikristo”. Kutoka hapa, Ukristo ulienezwa katika Afrika ya Mashariki.