
Delphine Froment
Mlima Kilimanjaro ni moja ya alama maarufu zaidi za utambulisho wa Tanzania. Ukiwa na urefu wa mita 5,895, ni mlima mrefu zaidi nchini na pia huitwa paa la Afrika, ukivutia wapenda kupanda milima kutoka pande zote za dunia. Mlima huu mkubwa ni alama inayoonekana kila mahali: kuanzia kauli mbiu ya shirika la ndege la Air Tanzania „The Wings of Kilimanjaro“, vivuko kati ya Dar es Salaam na Zanzibar vilivyopewa jina lake, hadi kwenye noti ya shilingi 5,000, nembo ya taifa, au bia ya Kilimanjaro Lager – kila mahali, Kilimanjaro huonekana kwa kilele chake maarufu kilichofunikwa na theluji na hugusa maisha ya umma.
Lakini umuhimu huu wa kiuchumi na kimaana unatokana moja kwa moja na jinsi Wazungu walivyoutazama mlima huo katika muktadha wa ukoloni na ubeberu – na baadaye wakaeneza mtazamo maalum juu ya namna ya kuuona na kuutumia mlima huo. Katika vitabu vya watalii, historia ya Kilimanjaro mara nyingi huanza mwaka 1848, wakati mmisionari Mjerumani Johannes Rebmann alipoelezwa kuwa “aliligundua” kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, “ugunduzi” huu ulikuwa wa Kizungu tu. Wachagga, waliokuwa wakiishi kwenye miteremko ya mlima huo, walikuwa tayari wanauelewa: Ingawa hawakuwahi kujaribu kufika kileleni, walipanda maeneo ya juu kwa ajili ya kuwinda na kukusanya, na walitumia misitu ya mlima huo kwa kazi mbalimbali kama vile kupikia, kujenga na ufugaji wa nyuki.
Aidha, Rebmann hakuenda peke yake – alisindikizwa na mwongoza njia na wabeba mizigo kutoka Pwani ya Waswahili, waliokuwa tayari wanaifahamu kanda hiyo. Kufikia katikati ya karne ya 19, Kilimanjaro ulikuwa kwenye makutano ya njia kuu za misafara zilizokuwa zimeendelea kwa miongo kadhaa, na hatimaye kuunganisha maeneo ya bara la Afrika ya Mashariki kuanzia pwani hadi kwenye maziwa makuu. Jina lenyewe “Kilimanjaro” huaminika linatokana na Pwani ya Kiswahili, ambapo Rebmann alilisikia kwa mara ya kwanza kabla ya safari yake mwaka 1848. Kiambishi “kilima” huchukuliwa kuwa ni Kiswahili kwa “mlima”, ilhali maana ya sehemu ya pili “njaro” bado inajadiliwa – baadhi ya mapendekezo ni kama “mlima wa ukubwa” au “mlima wa roho mbaya”. Wachagga waliokutana na “wagunduzi” wa kwanza walionekana kutolitumia jina hilo, bali waliutaja kwa jina la sehemu ya mlima, yaani Kibo, linalotumika hadi leo kwa kilele kikuu.

Hata hivyo, “ugunduzi” huu ulizua mshangao barani Ulaya: taarifa ya Rebmann ilizusha mjadala kuhusu kuwepo kwa theluji kwenye mlima huo – mjadala uliotatuliwa mwaka 1862. Taarifa hiyo ilichochea wimbi kubwa la uchunguzi Afrika Mashariki, eneo ambalo hadi wakati huo lilikuwa miongoni mwa sehemu zisizotembelewa sana na Wazungu. Kufikia mwisho wa miaka ya 1880, karibu msafara 15 ulikuwa umejaribu kufika kileleni – hakuna ulioweza kufanikisha, lakini wengi walishangazwa na ustawi wa Wachagga, jambo lililochochea tamaa ya ukoloni.
Katikati ya miaka ya 1880, Ujerumani na Uingereza waligombania Kilimanjaro, ambao hatimaye ulikuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (German East Africa). Mpaka wa sasa kati ya Kenya na Tanzania ni ushahidi wa migogoro hiyo ya kikoloni: Ingawa mstari wa mpaka huo unaanzia baharini hadi Ziwa Viktoria kwa mstari ulionyooka, unapinduka kwa makusudi karibu na Kilimanjaro – kutokana na umuhimu wa mlima huo kiusalama na kisiasa. Kati ya mvutano huo, mnamo mwaka 1889, mtafiti Mjerumani Hans Meyer alikuwa wa kwanza kufika kileleni. Alikiita kilele hicho “Kaiser-Wilhelm-Spitze” kwa heshima ya Mfalme wa Ujerumani, akaondoka na kipande cha jiwe kutoka kileleni, na kwa hivyo akaimarisha uwepo wa Kijerumani juu ya paa la Afrika.
Wakati wa ukoloni, Kilimanjaro iligeuka kuwa kitovu cha uchumi na eneo la ushawishi wa Ulaya Afrika Mashariki. Hali ya hewa nzuri na rasilimali nyingi ziliwavutia wamisionari, maafisa wa serikali na wakoloni. Sekta ya kahawa ilinawiri katika eneo hilo. Kufikia miaka ya 1910, barabara iliyopigwa lami, reli, na telegrafu zilikuwa zimeunganisha Kilimanjaro na mji wa Tanga kwenye pwani – jambo lililolifanya eneo hilo kuwa moja ya maeneo yaliyounganishwa zaidi na uchumi wa dunia. Wakati huohuo, Kilimanjaro ilianza pia kuvutia watalii – wakiwa na ndoto ya kuupanda au kuuona mlima wakati wa safari za mbugani. Utalii huu ulidhihirika kwa uwekezaji katika mahoteli, kuanzishwa kwa klabu ya wapandaji milima (Kilimandscharo Bergverein, 1913), na njia rasmi ya kupanda mlima, iliyokuwa na vibanda vya kupumzikia njiani.

Hata hivyo, utalii huo ulibaki kuwa wa kikundi kidogo cha watu matajiri: kulikuwa na mahoteli matatu tu kufikia mwisho wa ukoloni wa Kijerumani, na kupanda mlima mara 100 tu wakati wa ukoloni wa Waingereza. Lakini jamii za Kiafrika hazikubaki watazamaji tu wa mtazamo huu wa Kizungu juu ya mlima. Wachagga walianza kutoka katika shughuli zao za kilimo na kuwa waongozaji, wabeba mizigo na wapishi wa watalii. Taratibu, waliiga mila za Kizungu za kupanda mlima – mfano muhimu ni tarehe 9 Desemba 1962, ambapo kikundi cha Watanganyika walipanda mlima na kufurahia mwaka mmoja wa Uhuru kwa kufungua bendera ya taifa na kuwasha mwenge kwenye kilele kilichopewa jina jipya: Uhuru Peak – yaani “Kilele cha Uhuru.”
Mbali na maana ya ishara hiyo, ambayo ilihusisha mlima huo na utambulisho wa taifa jipya, Kilimanjaro ilianza kupewa nafasi rasmi katika sera za utalii za Tanzania kuanzia miaka ya 1970. Uwanja wa ndege wa kimataifa ulijengwa Arusha mwaka 1971, na Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro ilianzishwa mwaka 1973, ikirithi jitihada za uhifadhi zilizoanzishwa na wakoloni, ikiwemo hifadhi za misitu. Hifadhi hiyo ilifunguliwa kwa umma mwaka 1977 kwa njia mpya za kupanda mlima na huduma zaidi, na kufikia karne ya 21, utalii mwingi ulikuwa umeanza rasmi. Leo hii, mlima huo hupokea karibu wageni 50,000 kila mwaka – ambapo 35,000 hujaribu kupanda, na hutoa mapato ya dola milioni 55 za Kimarekani kwa mwaka.
Lakini kuwa chanzo kikuu cha utalii kumeenda sambamba na kunyang’anywa kwa jamii za haki zao za jadi, hasa kuanzia eneo la msitu wa mlima (msudu) kwenda juu. Juu ya mita 2,000, matumizi ya mlima huo sasa yamewekewa kikomo kwa aina fulani ya matumizi ya kibiashara – yaliyotokana na mfumo wa kikoloni na viwango vya Kizungu vilivyowekwa ili kuhudumia maslahi ya Kizungu. Wachagga wanakubalika tu kama watajibika kwa mfumo huo.
Matumizi mengine ya mlima na jamii za ndani hayaonekani. Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi endapo mradi wa njia ya kamba (cable car) utatekelezwa. Mradi huu, uliopendekezwa tangu 2019, unalenga kuwapeleka watalii hadi urefu wa mita 3,700 kwa dakika 30 tu, na hivyo kupunguza muda wa kupanda kwa kiasi kikubwa.
Ingawa mradi huo unaweza kuwasaidia watalii kutimiza ndoto zao za kupanda mlima, unahatarisha pia kuharibu mfumo wa kiuchumi wa ndani ambao watu wengi wa eneo hilo wanategemea. Kuondolewa kwa baadhi ya makundi ya watu (hasa Watanzania) kwa faida ya wengine (hasa Wazungu) ni muendelezo wa mienendo ya kihistoria inayoanzia nyakati za ubeberu.

Taarifa zaidi
- Wimmelbücker, Ludger (2002): Kilimanjaro. A Regional History. Production and Living Conditions, c. 1800-1920, Münster, Lit Verlag.
- Bender, Matthew V. (2019): Water Brings No Harm. Management Knowledge and the Struggle for the Waters of Kilimanjaro, Athens, Ohio University Press.
- Clack, Timothy A. R. (2007): Memory and the Mountain. Environmental Relations of the Wachagga of Kilimanjaro and Implications for Landscape Archeology, Oxford, Archeopress.
- Clack, Timothy A. R. (ed.), 2009, Culture, History and Identity: Landscapes of Inhabitation in the Mount Kilimanjaro Area, Tanzania. Oxford, Archeopress.
- Hamann, Christof & Honold, Alexander (2011): Kilimandscharo – die deutsche Geschichte eines afrikanischen Berges. Berlin, Verlag Klaus Wagenbach.