
Msafara wa Tendaguru huko Lindi: Historia ya Mabaki ya Mifupa ya Dinosauri, Mjadala wa Kurudishwa kwake, na Mahusiano ya Sasa
Acquillina Melchior Rweyemamu
Msafara wa Tendaguru (1909–1913) ulikuwa ni msafara mkubwa wa kipalontojia katika karne ya 20. Uliongozwa na wanasayansi wa Kijerumani, ndani ya Tendaguru katika mkoa wa Lindi, kusini mwa Tanzania (zamani Koloni la Ujerumani Afrika ya Mashariki). Mhandisi wa Kijerumani Bernhard Sattler, aliyekuwa mkurugenzi wa Kampuni ya Lindi Prospecting (Schürfgesellschaft), akiwa anatafuta madini kwajili ya kuokoa kampuni yake baada ya vita vya majimaji, alipata mifupa ya dinosauria baada ya kuongozwa na wenyeji wa Kitanzania mahali ilipo. Zaidi ya tani 225 za mabaki ya mifupa ilichimbwa na kupelekwa Ujerumani, ikiwemo mifupa ya Giraffatitan brancai ambayo bado inahifadhiwa katika Makumbusho ya Museum für Naturkunde, Berlin.
Wakati mabaki ya mifupa hiyo, inaenziwa kama mafanikio ya kisayansi nchini Ujerumani, uchimbaji wake ulitegemea nguvu kazi ya Watanzania,waliokuwa wakifanyakazi kwa kulazimishwa, na mchango wao kutokutambuliwa. Tangu mwanzo, Mabaki haya ya mifupa huelezwa kwa mitazamo ya watu wa Ulaya,bila kuzingatia historia ya ukoloni na umuhimu wa eneo hilo kwa jamii za Kitanzania. Kwa Watanzania wengi, msafara huo unaashiria unyonyaji wa kikoloni, upotevu wa tamaduni na ukosefu wa haki za kiuchumi. Hivi karibuni, kumekuwa na mijadala mingi kuhusu kuondoa athari za ukoloni katika makumbusho, kama ilivyoainishwa katika ripoti ya Sarr na Savoy ya mwaka 2018, ambayo inatoa wito wa kurejeshwa kwa vitu vya kale na vitu vya kikoloni vya Kiafrika. Pia kuwe na ushirikiano zaidi kati ya makumbusho na jamii za wenyeji.
Madai ya Marejesho na Changamoto Zake
Urejeshwaji wa ya mabaki ya mifupa ya Tendaguru bado ni suala tata na ambalo halijapatiwa suluhisho rasmi. Ingawa hakuna urejeshaji wowote rasmi uliofanyika hadi sasa, mazungumzo kuhusu suala hilo yanaendelea kushika kasi. Japokuwa Tanzania haijawasilisha madai rasmi ya urejeshaji, viongozi wake, vyombo vya habari, wanasiasa na jamii za wenyeji wameendelea kushinikiza kurejeshwa kwa vitu vya kitamaduni na kihistoria, wakisisitiza dhuluma za kihistoria na Mabishano ya umiliki.Serikali ya Tanzania imekuwa ikisita kuchukua hatua rasmi za kudai urejeshwaji, mara nyingi ikitaja ukosefu wa miundombinu na rasilimali za kuhifadhi Mabaki hayo ya mifupa, jambo ambalo ni la msingi. Hata hivyo, mwaka 2020, afisa mmoja wa serikali aliyetaka uwazi kuhusu asili ya mabaki ya mifupa na kuanzisha mjadala kuhusu urejeshwaji wake. Pia wasomi wamependekeza mbinu mbadala kama vile maonesho ya pamoja yanayoshirikisha pande zote, uzalishaji wa maarifa wa pamoja, Ubadilishanaji wa mafunzo na Maonyesho kwa njia ya simu, and urejeshwaji kwa njia ya kidijitali, ambao hutoa fursa ya upatikanaji wa mabaki ya mifupa na simulizi zake kwa njia ya mtandao. Mambo haya yote yangesaidia kuendeleza ushirikiano wa kitamaduni ulio wa haki zaidi. Wakati huohuo, makumbusho ya Ujerumani yanakumbwa na changamoto za kisheria na kisiasa, kwani mabaki ya mifupa hiyo mara nyingi hutambuliwa kama mali ya kisayansi ya kitaifa na mabaki ya binadamu.
Hali Halisi: Tupo Wapi Sasa?

Hadi sasa, mwaka 2025, Mabaki ya mifupa ya Tendaguru bado yapo Berlin licha ya shinikizo la kimataifa la kuirudisha. Baadhi ya vitu vya kale vya Kiafrika kama mabaki ya binadamu na vitu vya kiimani tayari vimesharudishwa kwa jamii husika, lakini si mifupa. Bado inaonekana kama rasilimali za kisayansi za kimataifa badala ya urithi wa kitamaduni. Hali hii imepelekea kuibuka kwa mijadala ya wazi zaidi kuhusu historia ya ukoloni. Makumbusho ya Museum für Naturkunde nchini Ujerumani imeanzisha programu za elimu na ziara kuhusu mada hii, huku Makumbusho ya Taifa ya Tanzania ikiendeleza ujenzi was kituo cha urithi huko Lindi na kuanzisha ushirikiano (www.nmt.go.tz/historical-centers/tendaguru-paleontological-site), ingawa bado inakumbwa na changamoto kama ukosefu wa fedha, miundombinu na utaalamu. Pamoja nayote haya, swali kubwa bado linabaki: Je, kutambuliwa kwa ishara tu kunatosha, au kurejeshwa kweli kunahitajika?
Kuelekea Maelewano ya Pamoja na Ushirikiano wa Tamaduni ujao
Marejesho ya maana yanahitaji usawa, mazungumzo endelevu na ushirikiano wa kweli. Makumbusho yanapaswa kuacha mienendo ya kikoloni na kushirikisha jamii husika tangu mwanzo. Ni jambo kubwa kuona hatua zinazochukuliwa na wataalamu wa Tanzania na Ujerumani wakifanya kazi pamoja, lakini wanapaswa kuhakikisha kwamba miradi hii inakuwa ya muda mrefu. Kwa Watanzania, Mifupa ya dinossaria inaonekana kuwa na thamani ya kiuchumi ambayoinaweza kusaidia kukuza ustawi wa jamii na kiuchumi, na pia inawakilisha utambulisho wa kitamaduni pamoja na maumivu ya ukoloni.
Hivyo basi, marejesho, hayapaswi kuwa ya kurudisha mifupa tu, bali yanapaswa kutambua kilichotokea, kuonyesha heshima na kubadilishana kwa usawa. Mifupa hii inaweza kusaidia kufanya makumbusho yawe mahali jumuishi, yenye uwajibikaji wa kimataifa na ushirikiano, badala ya kuwa vitu vya kikoloni vinavyohifadhi kumbukumbu za ukoloni.
Taarifa zaidi
- Chami, Maximilian Felix, Ndyanabo, Adson Samwel & Stoecker, Holger (2025): Finding Solutions for Managing, Protecting, and Promoting Tendaguru Palaeontological Site in Tanzania. In: Geoheritage 17, 44 (2025), online: https://doi.org/10.1007/s12371-025-01092-7
- Heumann, Ina, Stoecker, Holger & Vennen, Mareike 2021: Vipande vya Dinosaria: Historia ya Msafara wa Kipalentolojia kwenda Tendaguru Tanzania, 1906-2018. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota / 2024: Deconstructing Dinosaurs. The History of the German Tendaguru Exhibition and Its Finds, 1906-2023, Leiden: Brill, online open access: www.brill.com/display/title/69712
- Nguyen, Thuy Ann (2022): Auf knochigem Boden, online: www.leibniz-magazin.de/alle-artikel/magazindetail/newsdetails/auf-knochigem-boden
- Podcast Geschichten aus der Geschichte (2020): Die Tendaguru-Expedition und das größte Dinosaurierskelett der Welt, Nr. 230, online: www.geschichte.fm/podcast/zs230/
- Virtual Access to Fossil and Archival Material From the German Tendaguru Expedition, online: https://www.museumfuernaturkunde.berlin/en/research/virtual-access-fossil-and-archival-material-german-tendaguru-expedition-1909-1913.