Decolonial Travel Guide Tanzania

LUSHOTO & USAMBARA

Henriette Seydel

Katika eneo lenye rutuba la milima ya Usambara, watu wa jamii za Pare, Buga na Shambaa – kama jina lao linavyopendekeza („shamba“) – wamekuwa wakijishughulisha na kilimo tangu zamani. Katika maeneo ambapo mfalme Kimweri, aliyejulikana pia kama Simba Mwene (yaani “Mfalme Simba”), alitawala sehemu kubwa ya ardhi, mwaka 1886 wakoloni Wajerumani walitumia nguvu na rushwa baada ya upinzani mkali kuiteka ardhi hiyo. Hao Wajerumaniwaliasisi mji uliokuwa ukijulikana kama “Wilhelmsthal,” ulipewa jina la mfalme wa Ujerumani (Kaiser). Katika Lushoto ya leo, bado kuna alama za kihistoria zinazoonyesha mabaki ya ukoloni wa Kijerumani: kama jengo la zamani la utawala wa wilaya (kwa kijerumani Bezirksamt), ofisi ya posta, na majumba ya mashamba katika mabonde yanayozunguka mji.

Leo hii, milima ya Usambara – mojawapo ya maeneo yenye viumbe wengi na tofauti zaidi duniani – ni kivutio kwa wapenzi wa mazingira na wapenda kufanya matembezi kwenye uoto wa asili: mathalani; misitu minene, maporomoko ya maji mazuri, mimea adimu ya kuvutia, na aina nadra za ndege vinaweza kuchunguzwa hapa.

Kahawa …

Kutokana na hali ya hewa ya wastani na udongo wake wenye rutuba, Lushoto na milima ya Usambara ilikuwa kivutio kwa wakoloni wa Ulaya. Wajerumani walivutiwa zaidi na maendeleo ya kiuchumi ya koloni, hasa katika bidhaa za kilimo za kuuza nje. Mwaka 1886, kampuni ya „Deutsch-Ostafrikanische Plantagengesellschaft“ (Kampuni ya Kikoloni ya Mashamba ya Afrika Mashariki ya Kijerumani) ilianzishwa. Kilimo kilifanyika kwenye udongo wenye rutuba na mashamba mengi yalianzishwa, ambapo wenyeji walilazimishwa kufanya kazi kwa nguvu na manyanyaso. Kwa mfano, Wajerumani walipanda katani, pamba na kahawa katika maeneo haya. Ili kupata mbao, sehemu kubwa ya msitu wa mvua ilikatwa. Kupitia reli ya Usambara, bidhaa hizi zilisafirishwa hadi Tanga au Dar es Salaam, na kutoka huko kwa meli kwenda Ujerumani.

… maua pia hayakuwa mbali…

Kama jina linavyopendekeza, ua maarufu lijulikanalo kama Usambaraveilchen (Usambara violet), ambalo linapendelewa sana kama mmea wa nyumbani nchini Ujerumani, pia linatoka Tanzania. Afisa wa kikoloni ajulikanaye kama Adalbert Emil Walter Le Tanneux von Saint Paul-Illaire alituma mbegu za maua haya kwenda Ujerumani, ambako zilitambulika rasmi na kuchapishwa katika majarida ya kitaalamu. Jina la kisayansi la mmea huo, Saintpaulia ionantha, linahusiana na “mgunduzi” wa Kijerumani, ambaye alijimilikisha uoto wa asili ya Afrika ya Mashariki (kwa kujifanya mgunduzi).

…na urithi mwingine wa Kibiolojia wa Kikoloni

Katika eneo la Amani, kusini mwa milima ya Usambara, Taasisi ya Utafiti wa Kibiolojia na Kilimo ya Amani ilianzishwa mwaka 1902. Ilikuwa mradi wa mfano wa wakoloni katika utafiti wa kisayansi katika fani kama sayansi ya wadudu (entomology), botania, parasitolojia, zoolojia, kilimo na misitu. Utafiti juu ya mimea ya chakula na ya matumizi ulifanywa kwa lengo kuu la kufanya koloni kuwa ya faida na yenye tija. Hata mwanabakteria mashuhuri Robert Koch alifanya utafiti wake hapa alipokuwa Afrika. Mchango wake katika tiba ya kikoloni ya magonjwa ya kitropiki ulikuwa na mbinu zenye utata, ikiwa ni pamoja na majaribio ya kikatili kwa binadamu – ambayo hadi leo hayajafanyiwa tathmini ya kina.

Taarifa zaidi
  • Heyden, Ulrich van der (2007): Koloniales Gedenken im Blumentopf: Das Usambara-Veilchen und sein „Entdecker“ aus Berlin, in: Ulrich van der Heyden und Joachim Zeller (Hrsg.): Kolonialismus hierzulande – Eine Spurensuche in Deutschland. 220–222. Erfurt: Sutton Verlag, 
  • Kreye, Lars (2021): »Deutscher Wald« in Afrika. Koloniale Konflikte um regenerative Ressourcen, Tansania 1892–1916, Göttingen: Vandenhoeck & Ruprecht.
  • P. Wenzel Geißler, Rene Gerrets, Ann H. Kelly, Peter Mangesho (2020): Amani – Auf den Spuren einer kolonialen Forschungsstation in Tansania, Bielefeld: Transcript-Verlag
  • Tanga Tourism Network Association (2011): Usambara Moutains & Lushoto, in: Tourism Guide for the Tanga Region, 64-81, online: www.tangatourism.org