Decolonial Travel Guide Tanzania

Serengeti, Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

Henriette Seydel

Tazama Serengeti kama neno lenyewe linavyovutia. Bali pia safari kwa Wanyama pori, madhari ya kuvutia, makundi ya tembo mbele ya Mlima Kilimanjaro, twiga wakiwa kwenye mandhari ya machweo ya jua n.k. Mambo haya yote yanaunda picha na mitazamo ya kitalii kuhusu Tanzania. Ni ukweli usiopingika kuwa, utalii unachukuliwa kuwa injini ya uchumi na kiinua mgongo; kwa mfano mapato ya viingilio vya hifadhi za taifa hufadhili shughuli za uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

Hifadhi za taifa ziliundwa wakati wa Wakati wa ukoloni wa Wajerumani na Waingereza. Makabila mbalimbali yalinyang’anywa ardhi, rasilimali na maeneo yao mazuri. Wanyamapori na mazingira ya asili yaligeuzwa kuwa mali ya kipekee kwa maafisa wa kikoloni, wawindaji na baadaye watalii. Unyang’anyi huu wa ardhi na rasilimali za asili unajulikana pia kwa lugha ya kiingereza kama “Green Grabbing” au “Ukoloni wa Kijani.”

Hifadhi ya kwanza ya wanyamapori katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ilianzishwa mwaka 1896 na gavana wa kikoloni wa Kijerumani Hermann von Wissmann katika eneo la Rufiji kusini-mashariki. Baada ya Vita vya Maji Maji, eneo hilo liliweza kupanuliwa kwa sababu kulikuwa kuna upungufu wa watu. Kutokana na vita vya Maji Maji, wakoloni walijibu upinzani kwa kuharibu vijiji na mashamba. Watu ambao hawakufa kwa njaa au ukatili walikimbia. Misitu iliongezeka na wanyamapori walirudi tena. Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ya sasa ilijulikana awali kama Selous, jina lililotokana na mwindaji maarufu wa Kiingereza Sir Frederick Selous.

Mfano mwingine wa kufukuzwa kwa watu waishio maeneo hayo ni eneo la Kreta ya Ngorongoro na Serengeti. Hapo awali, tangu karne ya 18 waliishi Wamaasai, Wabarabaig na Wasonjo. Mwaka 1904, mkulima Mjerumani Adolf Siedentopf alianza shughuli za ufugaji na kilimo katika eneo hilo. Wenyeji walilazimishwa kuondoka au walilazimishwa kufanya kazi katika shamba hilo. Mabaki ya kuta na ngazi bado yanaonekana hadi leo. Mwanahistoria Bernhard Gissibl anaita magofu hayo kuwa ni jiwe la kukumbusha historia ya mwanadamu katika paradiso ya asili inayoonekana kana kwamba haijaguswa.

Utangazaji wa utalii kwa kutumia picha za kile kilichotwa “pori la kweli”

A lioness in the not entirely deserted wilderness (c) Magdalena Kula Manchee / Unsplash

Tangu miaka ya 1950, mwanzo wa kile kilichoitwa “Utalii wa Dunia ya Tatu,” picha ya Serengeti kama hifadhi ya paradiso ya wanyama bila binadamu ilianza kutangazwa. Waafrika walionekana tu kama mapambo ya hizi safari kama vile waongozaji watalii, wafanyakazi wa hoteli au kwa picha za kumbukumbu. Mchango mkubwa katika kuunda taswira hii ya asili ya kupendeza ulikuwa wa mwanasayansi maarufu wa Kijerumani, Bernhard Grzimek (“Serengeti isiangamie”), ambaye katika miaka ya 50 alihimiza maeneo ya hifadhi yasiyo na watu na alitetea “uhamisho wa hiari” wa wenyeji.

Uhamishaji wa watu kwa nguvu  kwa kupitia jina la uhifadhi na utalii bado unaendelea hadi leo

Ili kufikia malengo ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira wakati wa mabadiliko ya tabianchi, serikali ya Tanzania inapanga kuongeza maeneo ya hifadhi kutoka asilimia 30 hadi 50 ya eneo lote la nchi. Hili linahitaji kuwahamisha watu wanaoishi katika maeneo hayo. Serikali inasema kwamba ongezeko la idadi ya watu linatishia mifumo nyeti ya mazingira kwa sababu ya kuongezeka kwa maeneo ya malisho na mifugo, jambo ambalo linapunguza makazi ya wanyamapori. Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kuwa jamii za asili mara chache huathiri mazingira kwa njia hasi. Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kwamba jamii za asili mara chache huathiri mazingira kwa njia hasi. Kinyume chake: maeneo ambako kwa mfano Wamaasai wanaishi mara nyingi yanaonyesha kuwa na aina nyingi za viumbe hai. Serikali ya Tanzania inazungumzia uhamisho wa hiari; nyumba mpya, miundombinu na shule zimetolewa, lakini mara nyingine zipo mamia ya kilomita mbali na makazi ya awali. Watu wengi wanaona hii “hiari” kwa mtazamo wa mashaka, kwani vikosi vya usalama, polisi na walinzi wa wanyamapori waliwafukuza Wamaasai kwa nguvu. Maandamano yalizimwa kwa ghasia, na waandamanaji wengine walikamatwa na kuwekwa kizuizini. Watu waliokumbwa na unyang’anyi wa ardhi, kufukuzwa na ukiukwaji wa haki zao za binadamu waliamua kufungua mashitaka mahakamani dhidi ya serikali ya Tanzania.

Muendelezo wa miundo ya kikoloni yenye ukosefu wa usawa

Wakosoaji wanaamini kuwa maslahi ya kiuchumi ndiyo yanayopewa kipaumbele madhalani, maeneo ya uwindaji, hoteli za kifahari na viwanja vya ndege vinapangwa kupanuliwa – kwa gharama ya jamii za wenyeji. Hii inaibua maswali kuhusu mantiki ya hatua hizo. Kuna utata mkubwa: inakuwaje Wamaasai walazimishwe kuondoka kwenye hifadhi za taifa kwa sababu za uhifadhi wa mazingira, lakini watu wengi zaidi waruhusiwe kuingia – wakiwemo wanaowinda wanyamapori wanaopaswa kulindwa? Na hayo yote yakifuatana na uchafuzi wa mazingira kupitia ndege, magari ya watalii (jeep), matumizi makubwa ya maji na ongezeko la taka? Inawezekanaje nyumba za Wamaasai, vituo vya afya au shule kwa ajili ya watoto wao vionekane kama tatizo kwa mazingira na wanyama, ilhali hoteli za nyota tano na maeneo ya kambi ya wageni haziwekwi katika mizani hiyo?

Na si jambo la kushangaza kwamba kunufaika na ongezeko la safari za utalii mara nyingi ni makampuni ya kigeni na wawekezaji wa nje zaidi ya jamii za wenyeji. Sehemu kubwa ya hoteli za safari na waendeshaji wa ziara si Waafrika, au wanamilikiwa na watu wa tabaka la juu wa Tanzania. Wafanyakazi kama waongozaji (guides), madereva au wapishi mara nyingi hufanya kazi katika mazingira ya kazi yasiyo na usalama wa ajira. Ingawa serikali ya Tanzania ina mpango wa kukuza utalii wa ndani, safari bado ni ghali na hivyo hazifikiwi na sehemu kubwa ya Watanzania.

Taarifa zaidi