Decolonial Travel Guide Tanzania

Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania

Constanze Menard

Kwa ujumla, kuna maeneo mengi ya kihistoria katika kanda ya kusini mwa Tanzania yenye uhusiano na historia ya ukoloni wa Kijerumani, ambayo mara nyingi hayahifadhiwi wala kufanyiwa tafiti ipasavyo. Vilevile, kuna upungufu mkubwa wa nyumba za makumbusho, utafiti na juhudi za kushughulikia historia hiyo katika eneo hili.

Maporomoko ya Maji ya Kimani

Katika hifadhi ya asili ya Mpanga-Kipengere kuna maporomoko makubwa ya maji ya Kimani, ambayo yanahusiana na maisha ya Chief Mkwawa. Chief Mkwawa alikuwa akifanya mikutano ya siri ya kijeshi katika eneo hili ambalo sasa limehifadhiwa, na kwa nyakati fulani alijificha kwenye mapango yaliyo karibu na maporomoko hayo. Eneo hili linapatikana kwa urahisi na linahifadhiwa vyema na walinzi wa hifadhi ambao pia hutoa maelezo na maelezo ya kihistoria kwa wageni.

Kidugala

Kijiji cha Kidugala ni mojawapo ya vituo vya zamani vya wamisionari wa Kijerumani, na kipo katika vilima vya milima ya Livingston. Majengo yote kama vile kanisa, shule ya zamani na nyumba ya kasisi bado yapo. Wakati wa Vita ya Pili ya Dunia, wakimbizi wa Kipolandi walihamishiwa kijijini hapa (rej. Mkataba wa Sikorski-Majski). Kuna maonyesho madogo ya kudumu kwenye eneo la kanisa yanayoeleza historia hiyo. Kwenye kumbukumbu za shule ya Biblia kunafanyiwa kazi na uchambuzi juu ya historia ya utume na ukoloni.

Rungwe Archive and Museum Centre (c) Moravian Church in Tanzania

Utengule (Njombe)

Katika kijiji hiki kuna mnara wa kihistoria unaokumbusha vita kati ya Wabena na Wajerumani.

Tukuyu

Mji huu ulianzishwa mwaka 1900 na watawala wa Kijerumani kwa jina la Neu Langenburg juu ya kilima. Kituo cha awali, Fort Langenburg (leo kinaitwa Lumbila), kiliharibiwa na kupotea kwa sababu ya kuongezeka kwa maji katika Ziwa Nyasa. Mji mpya uliipa kanda nzima jina la Langenburg na kuwa kitovu muhimu cha siasa za kikanda.

German Fort in Tukuyu (c) Kathleen Bomani

Kisiba

Kilomita chache kutoka Tukuyu kuna Ziwa la Kasoko la Kisiba, ambapo kuna majengo ya zamani ya Boma ya Kijerumani, mengine bado yanatumika na mengine yamechakaa. Katika ziwa hili dogo lakini refu sana, unaweza kuogelea kwa usalama. Kulingana na simulizi, baada ya kuzuka kwa vita, wanajeshi wa Kijerumani waliondoka/kukimbia kutoka eneo hili na kutupa ndani ya ziwa mali yote ambayo haikuweza kubebwa na ambayo hawakutaka iangukie mikononi mwa Waingereza. Hadi miaka ya 1980, sarafu za shaba zilisemekana kuwa bado zinapatikana.

Musomba

Pia katika Tukuyu kuna makao makuu ya Jumuiya ya Ndugu wa Herrnhut na KMKT kwa kanda ya Rungwe na kusini mwa Tanzania. Tangu mwaka 1991, kuna mradi wa makumbusho na kumbukumbu ambao unahifadhi historia ya utume wa Herrnhut, historia ya nyanda za juu kusini na jamii za wenyeji kupitia nyaraka na picha.

Liuli (Ruvuma)

Ni mji uliopo karibu na Ziwa Malawi, ambao uliitwa Sphinxhafen na wakoloni wa Kijerumani, na ulitumika kama bandari ya kuanzia kwa ajili ya kuendeleza ukoloni katika nyanda za juu kusini. Njia ya nchi ilikuwa haipitiki kwa sababu ya mapambano ya Wahehe. Jina “Sphinx” linatokana na miamba saba ya ajabu iliyoko ndani ya maji. Sphinxhafen ni maarufu kwa kuwa eneo la kwanza ambapo Jeshi la Majini la Ujerumani lilifanya operesheni wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia.